Thursday, March 8, 2012

MANJI AKANUSHA KUJIHUSISHA NA KUING'OA SIMON GROUP KUMILIKI UDA

SAKATA la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kubinafsishwa, limeingia sura nyingine baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji wa Quality Group, kujitokeza na kutoa taarifa kuhusu upande wake na UDA.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ikiwa ni saa kadhaa tu baada ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi naye kutoa yake, Manji alitaka asizongwe kuhusu ubinafsishaji wa shirika hilo, ambao unahusisha pia kampuni ya Simon Group ambayo hivi karibuni iliingiza nchini mabasi yapatayo 40.

Manji katika taarifa yake anakanusha kujihusisha na ufadhili wa harakati za kutaka kuing’oa Simon Group katika umiliki wa UDA.

“Taarifa za hivi karibuni za vyombo vya habari, zinajaribu kuelezea kwamba mimi ndiye nimekuwa kinara wa kuratibu harakati za viongozi wa Dar es Salaam wanaohoji uhalali wa ubinafsishaji wa UDA kwa sababu eti wengi ni rafiki zangu,” alisema Manji.

Amekiri katika taarifa hiyo kwamba aliposikia taarifa kwamba UDA imebinafsishwa kwa Simon Group, aliwaandikia wenyeviti wa kamati mbili za kudumu za Bunge zenye majukumu ya uangalizi wa mashirika ya umma.

“Niliandika barua kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma, nikiomba ufafanuzi juu ya taratibu zilizotumika kulibinafsisha shirika hili,” alisema na kuongeza kuwa Quality Group ilishiriki katika zabuni mbili; ya mwaka 2007 ilijitokeza kama mwombaji pekee.

Alisema katika zabuni hiyo walikuwa tayari kuingia ubia kwa Sh. bilioni 1.50 ili kununua hisa 49 za UDA na kukubali kuwekeza dola milioni 10 za ukarabati wa karakana na kuleta mabasi 150 chini ya utaratibu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam (DART). Hata hivyo hawakujibiwa.

Katika taarifa hiyo, Manji alifafanua kuwa waliandika barua kutaka kujua udhaifu wao ili siku za usoni wajirekebishe na ndiyo sababu kamati hizo za Bunge zikaibuka kutaka kuulizia suala hilo katika mamlaka husika –Wizara ya Fedha.
“Walichoomba wenyeviti hao ni taarifa au maelezo ya mchakato wa ubinafsishaji wa shirika … ni baada ya ombi letu la Agosti 14, 2007 kutojibiwa … haikuwahi kutangazwa tena zabuni ya ubinafsishaji mpaka tuliposoma magazetini, kwamba shirika tayari limebinafsishwa kwa Simon Group.

Manji katika taarifa yake anasema mkataba wa mwisho wa upangishaji wa eneo hilo ulifanywa mwaka jana chini ya makubaliano ya ukodishaji ambapo Quality Group ililipa kodi ya miaka mitatu kwenye akaunti ya UDA, kabla ya kuanza kupangisha na si “kwenye akaunti ya mtu kama alivyofanya Simon Group.”

Kwa upande wake, Dk Masaburi nayae anakanusha kuhusika na njama za kutoa dola 133,125 za UDA ingawa anakiri kuidhinisha utoaji wa Sh 51,616,748 za Simon Group kwa ajili ya mishahara, kulingana na makubaliano kuwa Simon Group iendelee kutumia UDA bila kufanya uamuzi mkubwa.

Umekuwapo mvutano mkubwa kati ya wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam na Dk Masaburi juu ya ubinafsiahaji wa UDA mpaka kutoleana maneno makali.
 
blog ya lukwangule

No comments:

Post a Comment