Thursday, March 8, 2012

MFAHAMU MGOMBEA JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI-KAMANDA JOSHUA NASARI

Joshua Nasari alizaliwa januari 8 mwaka 1985 katika kijiji cha Kilinga Meru, Wilayani Arumeru kwenye hospitali ya Nkoaranga.
Wagombea waliokuwa wanagombea na Joshua Nasari ni Anna Mughwira ambaye ni Mwanasheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Makumira, Katibu wa baraza Vijana wa Chama hicho Wilayani Arumeru, Godlove Ismail Temba, Yohane Kimunto, Samweli Shamy na Rebeca Magwisha.

Kijana huyu anazungumza kuwa yeye ni mmoja kati ya watoto nane wa Mchungaji Samweli Nassari, kati ya hao watoto watano ni wakiume watatu na watoto watano wanawake, ambapo yeye ni wa pili kwa upande wa watoto wa kiume na katika nafasi ya kuzaliwa ni watano.
Anasema elimu yake ya msingi aliipata shule ya msingi Mulala iliyopo huko Meru kuanzia mwaka 1993 kuhitimu mwaka 1999, ambapo mwaka 2000 alijiunga na masomo ya Sekondari Bagamoyo na kuhitimu mwaka 2003.

Nassari anasema mwaka 2004 alijiunga na masomo ya Sekondari ya kidato cha tano shule ya Sekondari Tabora na kumaliza masomo hayo mwaka 2006 na baada ya hapo alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Augusti mwaka 2009 alihitimu masomo yake na kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Jamii, katika Masuala ya utengenezaji Sera na Utawala.
Aidha anasema baada ya hapo aliendelea kujiendeleza ambapo mwaka 2011 alipata kozi katika Chuo cha Mafunzo cha Ushirikiano wa Maendeleo (MS-TCDC) ambako alisomea haki za watoto na utetezi

Uzoefu katika kazi Joshua Nassari anasema mwaka 2009 hadi 2012 alishafanya kazi kwenye shirika la Kimarekani la Foundation For Tommorow, lenye tawi lake Mkoani Arusha na alikuwa Mkurugenzi wa Mipango.
“Mimi ninauzoefu wa kuwa Meneja katika ofisi ya Shirika la Amend. Org la Jijini Dar es Salaam nchni Tanzania ambako nilifanya kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2009 na Machi 2008 nilifanya utafiti kuhusu mtazamo wa Afya ya watoto, ambapo niangalia zaidi suala la watoto yatima na watoto wa mitaani,” anasema Nassari.
Nassari anasema kuwa uzoefu mwingine alionao mbali na huo, alishawahi kufanya utafiti wa Kimataifa Chuo Kikuu cha Dartmounth kilichopo nchini Marekani na pia alifanya utafiti kwa waganga wa jadi, wafanyakazi waponyaji wa Afya wanaojishughulisha na utunzaji wa Afya za watoto Vijijini, hayo aliyafanya mwaka 2008 katika mwezi wa nane na tisa.
Mgombea huyu hakuishia hapo tu, kwa miezi mitatu mwaka 2008 alifanya utafiti katika shirika la Surpport for International Change lililopo Jijini Arusha na alishawahi kuwa mwalimu mshiriki katika mwezi Machi, Mei 2006 na Juni na Julai 2007 alifanya kazi shirika la Global Service Corps,lakini wakati huo alikuwa akiendelea kusoma Chuo Kikuu cha Da es Salaam.
Uzoefu kwa upande wa Kisiasa anasema, Desemba 10 mwaka 2012 hadi sasa, anafanya kazi katika ofisi za Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye shirika la Arusha Devolopment Foundation (ARDF) na Agosti hadi Oktoba mwaka 2010 alikuwa mgombea katika nafasi ya Ungunge Jimbo la Arumeru Mshariki kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.
Anasema pia uzoefu mwingine wa kuwa kiongozi, alishawahi kuwa Spika wa Bunge la Wanafaunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO), mwaka 2008 alikuwa Mbunge wa Bunge kivuli wa Vijana wa umoja wa Mataifa.
Anasema shughuli zingine alizofanya akiwa Chuoni ni kujiunga klabu na Aprili hadi Julai 2009 alikuwa Rais wa Shirika la Wanafunzi la Kimataifa linaloshughulikia kampeni dhidi ya Ukimwi na Oktoba hadi Julai 2009 alikuwa Rais wa shirika la Save Albino.Com la kutetea Albino.
Nassari anasema kuwa msukumo mkubwa uliomsukuma kujikita katika siasa na kufikiria kuacha kazi shirika la Marekani la Foundatino for Tommorow, ili kujipa nafasi kubwa ya kufanya kampeni katika kuhakikisha anashinda Jimbo hilo na kuwawakilisha wananchi ni uchungu alionao kwa wakazi wa Jimbo hilo.
Anasema kuwa tangu Uhuru Jimbo hilo linashikiliwa na Chama cha Mapinduzi, lakini hakuna maendeleo yoyote waliyofanya, zaidi ya kuwaacha wakazi wa Jimbo hilo wakinyang’anywa ardhi yao sehemu kubwa na kupewa Masetla na maeneo ya maji ambayo yapo mengi katika Jimbo hilo hayawanufaishi wakazi hao.
“Mimi nikifanikiwa kupata Jimbo hili, nitahakikisha natatua kero hizi, sababu uzoefu wa kufanya kazi za jamii ninao na jinsi ya kutafuta fedha za kuendesha miradi upo,”anasema Nassari.
Nassari anasema kuwa wakazi wa Arumeru Mashariki wanahitaji mtu wa kuwatetea na kuwasemea kero zao bungeni na siyo kupata mtu wa kujijali yeye na familia yake na kuwaacha wakazi hao wakipata shida miaka nenda rudi.
Aidha, Nassari ameapa kuhakikisha mara tu atakapoingia madarakani, kuhakikisha maeneo yote yaliyomezwa na na kumilikiwa kinyemela na Masetla anayapigania na kuyarudisha mikononi mwa wananchi.
Nassari anasema wananchi wa Jimbo hilo wengi wao wanahitaji tumaini jipya kutoka kwa mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na siyo vinginevyo.
Kijana huyo Machachari, akiongea hayo huku akijiamini na kuungwa mkono na maelfu ya wakazi wa Jimbo hilo, anasema kwanza tayari ana mtaji wa watu 29,000, hivyo hawezi kushidwa kunyakua Jimbo, kwa sababu kazi iliyopo ndogo ya kuwasaka wengine wachache kujaza hapo.
Nassari anasema wakati wa sasa wa kuziamini na kuzifuata propaganda chafu, umepitwa na wakati, hivyo wananchi wa Jimbo hilo wanahitaji Propoganda safi na zinazotekelezeka na sio kurubuniwa kwa fedha na tisheti.
Uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa Jimbo la Arusha na kuzua zogo Jijini Arusha, huku baadhi ya magari ya daladala yakianza kupeperusha bendera za Chadema hasa zile za kwenda Usa River na Kikatiti, utakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na Chadema

No comments:

Post a Comment