Thursday, March 8, 2012

MGOMO WA MADAKTARI:TUSIDHARAU WAKUNGA NA UZAZI UNGALIPO-PROF MBELE

Niko Dar es Salaam, kuanzia Machi 3, na kuanzia siku mbili zilizopita, kumekuwa na mgomo wa madaktari, kufuatia madai yao kuwa serikali haijatekeleza makubaliano yaliiyofikiwa wiki chache zilizopita. Nimesikiliza kauli za Waziri Mkuu Pinda pia.

Ninachoweza kusema, kwa ufupi kabisa ni kuwa serikali ya Tanzania imeamua kukiuka busara ya wahenga kwamba tusidharau wakunga na uzazi ungalipo. Ni jambo la ajabu na la kutisha kwa serikali au nchi kugombana na madaktari. Kwamba Tanzania imefikia hapo ni dalili tosha za kutowepo busara za kiuongozi.

Madai ya madaktari, tangu mwanzo nayaafiki. Madai hayo ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi mahospitalini, uwepo wa vifaa, madawa, na kadhalika. Vipato vya madaktari navyo ni duni sana. Tafsiri yangu ni kuwa madai ya madaktari hayahusu maslahi yao binafsi tu, bali maslahi ya wagonjwa. Tanzania, nchi yenye rasilimali nyingi, yenye serikali ambayo inafuja mali kwa namna mbali mbali, inaweza kabisa kutekeleza madai ya madaktari.

Nitoe mfano moja tu wa ufujaji unaofanywa na serikali. Wakati serikali hii ilipoanza kazi, Waziri Mkuu Pinda aliliambia Taifa kuwa alikuwa amenunuliwa gari la bei kubwa sana, na kwamba kutokana hilo, hakuwa tayari kulitumia. Binafsi najiuliza: je, waliofanya uamuzi wa kununua hilo gari waliwajibishwa? Na je, gari la fahari lililonunuliwa ni hilo moja tu? Na je, kwa nini serikali ya Tanzania isipige marufuku magari ya fahari? Nasikia Rwanda walishapiga marufuku magari hayo. Kwa nini serikali ya Tanzania isifanye hivyo hivyo. Huo ni mfano moja tu, lakini ningeweza kuandika zaidi.

Sote tunakubaliana na kuwa kazi ya udaktari ni nyeti kabisa, kwa maana kwamba inahusu uhai wa binadamu moja kwa moja. Hilo suala la unyeti wa shughuli za madaktari lilisisitizwa na Waziri Mkuu Pinda katika hotuba yake wiki hii. Hakuna ubishi hapo. Sasa basi inabidi tukubaliane kuwa ni muhimu maslahi ya madaktari ni lazima yawekwe mbele kuliko ilivyo sasa. Ni hatari kwa maisha yetu iwapo madaktari wako kazini huku wakihofia kodi ya umeme watalipaje au watoto wao watakula nini. Tufanye kila liwezekanalo ili daktari akiwa kazini, awe pale kwa roho moja, akitoa tiba.

Madaktari wamesema hawana imani na viongozi wawili wa wizara ya afya. Inashangaza kuona serikali ikipuuzia jambo hilo na kuliendesha kiubabe. Busara za kiuongozi zinaeleza kuwa morali ya watu ni jambo muhimu sana. Morali ya madaktari ingekuwa juu iwapo wangetekelezewa dai lao kuhusu kuondolewa kwa viongozi hao wa wizara.

Lakini serikali imeamua kuwakingia kifua watu wawili na hivi kudidimiza morali ya jumuia kubwa ya madaktari. Halafu, serikali inajaribu kujenga hoja kuwa madaktari hawathamini uhai wa wananchi. Hoja hii imenishangaza.

Kama kuna ambaye hathamini uhai wa wa-Tanzania ni serikali tuliyo nayo. Serikali hii imeacha wazi mianya ya rasilimali ya Taifa kuporwa, wakati rasilimali hii ingeweza kutumiwa kuokoa maisha ya watu mahospitalini kwa kununulia madawa na vifaa mbali mbali. Serikali inayofumbia macho ufisadi ndio mhujumu wa maisha ya wa-Tanzania. Hainiingii akilini kuwa serikali hii inajaribu kujifanya ndiyo ina uchungu na maisha ya wa-Tanzania.

Mambo mengine ya serikali hii yanachekesha. Pakitokea maandamano, kuanzia chuo kikuu hadi Songea, tunashuhudia jinsi polisi wanavyorusha mabomu na hata risasi. Hakuna siku tukasikia kuwa kuna upungufu wa mabomu na risasi. Serikali imewekeza katika mabomu ya kuwalipulia wananchi, wakati huduma za hospitali zina walakini. Ni ajabu na kweli.

via blogu ya Prof. Mbele

MFAHAMU MGOMBEA JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI-KAMANDA JOSHUA NASARI

Joshua Nasari alizaliwa januari 8 mwaka 1985 katika kijiji cha Kilinga Meru, Wilayani Arumeru kwenye hospitali ya Nkoaranga.
Wagombea waliokuwa wanagombea na Joshua Nasari ni Anna Mughwira ambaye ni Mwanasheria katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Makumira, Katibu wa baraza Vijana wa Chama hicho Wilayani Arumeru, Godlove Ismail Temba, Yohane Kimunto, Samweli Shamy na Rebeca Magwisha.

Kijana huyu anazungumza kuwa yeye ni mmoja kati ya watoto nane wa Mchungaji Samweli Nassari, kati ya hao watoto watano ni wakiume watatu na watoto watano wanawake, ambapo yeye ni wa pili kwa upande wa watoto wa kiume na katika nafasi ya kuzaliwa ni watano.
Anasema elimu yake ya msingi aliipata shule ya msingi Mulala iliyopo huko Meru kuanzia mwaka 1993 kuhitimu mwaka 1999, ambapo mwaka 2000 alijiunga na masomo ya Sekondari Bagamoyo na kuhitimu mwaka 2003.

Nassari anasema mwaka 2004 alijiunga na masomo ya Sekondari ya kidato cha tano shule ya Sekondari Tabora na kumaliza masomo hayo mwaka 2006 na baada ya hapo alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Augusti mwaka 2009 alihitimu masomo yake na kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Jamii, katika Masuala ya utengenezaji Sera na Utawala.
Aidha anasema baada ya hapo aliendelea kujiendeleza ambapo mwaka 2011 alipata kozi katika Chuo cha Mafunzo cha Ushirikiano wa Maendeleo (MS-TCDC) ambako alisomea haki za watoto na utetezi

Uzoefu katika kazi Joshua Nassari anasema mwaka 2009 hadi 2012 alishafanya kazi kwenye shirika la Kimarekani la Foundation For Tommorow, lenye tawi lake Mkoani Arusha na alikuwa Mkurugenzi wa Mipango.
“Mimi ninauzoefu wa kuwa Meneja katika ofisi ya Shirika la Amend. Org la Jijini Dar es Salaam nchni Tanzania ambako nilifanya kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2009 na Machi 2008 nilifanya utafiti kuhusu mtazamo wa Afya ya watoto, ambapo niangalia zaidi suala la watoto yatima na watoto wa mitaani,” anasema Nassari.
Nassari anasema kuwa uzoefu mwingine alionao mbali na huo, alishawahi kufanya utafiti wa Kimataifa Chuo Kikuu cha Dartmounth kilichopo nchini Marekani na pia alifanya utafiti kwa waganga wa jadi, wafanyakazi waponyaji wa Afya wanaojishughulisha na utunzaji wa Afya za watoto Vijijini, hayo aliyafanya mwaka 2008 katika mwezi wa nane na tisa.
Mgombea huyu hakuishia hapo tu, kwa miezi mitatu mwaka 2008 alifanya utafiti katika shirika la Surpport for International Change lililopo Jijini Arusha na alishawahi kuwa mwalimu mshiriki katika mwezi Machi, Mei 2006 na Juni na Julai 2007 alifanya kazi shirika la Global Service Corps,lakini wakati huo alikuwa akiendelea kusoma Chuo Kikuu cha Da es Salaam.
Uzoefu kwa upande wa Kisiasa anasema, Desemba 10 mwaka 2012 hadi sasa, anafanya kazi katika ofisi za Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye shirika la Arusha Devolopment Foundation (ARDF) na Agosti hadi Oktoba mwaka 2010 alikuwa mgombea katika nafasi ya Ungunge Jimbo la Arumeru Mshariki kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.
Anasema pia uzoefu mwingine wa kuwa kiongozi, alishawahi kuwa Spika wa Bunge la Wanafaunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (DARUSO), mwaka 2008 alikuwa Mbunge wa Bunge kivuli wa Vijana wa umoja wa Mataifa.
Anasema shughuli zingine alizofanya akiwa Chuoni ni kujiunga klabu na Aprili hadi Julai 2009 alikuwa Rais wa Shirika la Wanafunzi la Kimataifa linaloshughulikia kampeni dhidi ya Ukimwi na Oktoba hadi Julai 2009 alikuwa Rais wa shirika la Save Albino.Com la kutetea Albino.
Nassari anasema kuwa msukumo mkubwa uliomsukuma kujikita katika siasa na kufikiria kuacha kazi shirika la Marekani la Foundatino for Tommorow, ili kujipa nafasi kubwa ya kufanya kampeni katika kuhakikisha anashinda Jimbo hilo na kuwawakilisha wananchi ni uchungu alionao kwa wakazi wa Jimbo hilo.
Anasema kuwa tangu Uhuru Jimbo hilo linashikiliwa na Chama cha Mapinduzi, lakini hakuna maendeleo yoyote waliyofanya, zaidi ya kuwaacha wakazi wa Jimbo hilo wakinyang’anywa ardhi yao sehemu kubwa na kupewa Masetla na maeneo ya maji ambayo yapo mengi katika Jimbo hilo hayawanufaishi wakazi hao.
“Mimi nikifanikiwa kupata Jimbo hili, nitahakikisha natatua kero hizi, sababu uzoefu wa kufanya kazi za jamii ninao na jinsi ya kutafuta fedha za kuendesha miradi upo,”anasema Nassari.
Nassari anasema kuwa wakazi wa Arumeru Mashariki wanahitaji mtu wa kuwatetea na kuwasemea kero zao bungeni na siyo kupata mtu wa kujijali yeye na familia yake na kuwaacha wakazi hao wakipata shida miaka nenda rudi.
Aidha, Nassari ameapa kuhakikisha mara tu atakapoingia madarakani, kuhakikisha maeneo yote yaliyomezwa na na kumilikiwa kinyemela na Masetla anayapigania na kuyarudisha mikononi mwa wananchi.
Nassari anasema wananchi wa Jimbo hilo wengi wao wanahitaji tumaini jipya kutoka kwa mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na siyo vinginevyo.
Kijana huyo Machachari, akiongea hayo huku akijiamini na kuungwa mkono na maelfu ya wakazi wa Jimbo hilo, anasema kwanza tayari ana mtaji wa watu 29,000, hivyo hawezi kushidwa kunyakua Jimbo, kwa sababu kazi iliyopo ndogo ya kuwasaka wengine wachache kujaza hapo.
Nassari anasema wakati wa sasa wa kuziamini na kuzifuata propaganda chafu, umepitwa na wakati, hivyo wananchi wa Jimbo hilo wanahitaji Propoganda safi na zinazotekelezeka na sio kurubuniwa kwa fedha na tisheti.
Uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa Jimbo la Arusha na kuzua zogo Jijini Arusha, huku baadhi ya magari ya daladala yakianza kupeperusha bendera za Chadema hasa zile za kwenda Usa River na Kikatiti, utakuwa wa ushindani mkali kati ya CCM na Chadema

Taarifa kwa vyombo vya Habari:Dkt Hamis Kigwangala akanusha kuutaka UWAZIRI

Thursday, March 8, 2012

OFISI YA MBUNGE, JIMBO LA NZEGA

Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (MB)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tunapenda kuutarifu umma kwamba Mhe. Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesikitishwa sana kupata taarifa kutoka baadhi ya vyombo vya habari kuwa anatajwa kuchochea mgomo wa madaktari. Hata siku moja hajawahi kuwa mchochezi wa mgomo huu na yeye binafsi siku zote amekuwa mstari wa mbele kusema ukweli na kuweka hadharani msimamo wake na wala siyo kuchochea kwa kificho chini kwa chini.

Pia kuna gazeti moja la kila wiki limeandika jana stori (kwenye ukurasa wake wa mbele) kuwa Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla ‘anatajwa kuchochea mgomo huo kwa malengo ya kuutaka uwaziri.’ Vyombo vingi vya habari vikivutiwa na kichwa hiki cha habari vimekuwa vikimpigia simu Mhe. Mbunge kumtaka atoe ufafanuzi. Mhe. Mbunge amesikitishwa sana na taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti hili na tayari Mwanasheria wake ameanza kujipanga kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulitaka gazeti hili limsafishe kwenye jamii kwa kuchapisha habari ya kumsafisha ama lipelekwe mahakamani.

Kwa taarifa hii tunakanusha ushiriki wa aina yoyote ile unaotajwa kumhusisha Mbunge wa Nzega kwenye uchochezi ama wa namna yoyote ile inayofikirika zaidi ya msimamo ambao Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla amewahi kuuweka wazi siku za nyuma kwenye mikutano ya wazi ya madaktari au kwenye vyombo vya habari.

Pia ifahamike kuwa kwa kuweka wazi msimamo wake kwamba madaktari wana madai ya msingi na hivyo wasikilizwe (ambayo kwa sasa serikali ilishakiri na kuyakubali madai yao na kutamka hadharani kuwa inayafanyia kazi) haimaanishi kuwa ni uchochezi bali ni matumizi ya haki za msingi za binadamu kama zilivyoainishwa kwenye Kati ba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye mikataba mbali mbali ya kimataifa ya haki za binadam.


Na pia tunapenda kuwataarifu wanahabari kuwa Dkt. Hamisi Kigwangalla hajahudhuria mkutano wowote ule wa madaktari uliopelekea madaktari kuazimia kugoma tena na hivyo kumhusisha na ushawishi ama uchochezi ni kupotosha umma na kuvunja sheria.

Na zaidi kufikiria kuwa madaktari nchi nzima wanaweza kugoma kwa kumsikiliza mtu mmoja tu ni kuwatukana na kuwadhalilisha kwa kuwaona hawana uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi yao, ilhali hawa ni watu makini, wenye elimu na ujuzi wa hali ya juu na wengi wao wanamshinda elimu, ujuzi na uzoefu kwa mbali sana Mhe. Mbunge Dkt. Kigwangalla.

Hali kadhalika, Mhe. Dkt. Kigwangalla aliomba Ubunge na hakutarajia kuwa angepewa Uwaziri na ni wazo la kitoto kufikiria kwamba mtu mwenye busara zake na hadhi yake kama yeye angeweza kupanga mkakati wa kumn’goa Waziri yeyote Yule ili awekwe yeye, maana kwanza hana muamana na mamlaka ya uteuzi, ambayo kimsingi ndiyo yenye uamuzi wa kumteua nani na kumuondoa nani, na pia haiyumkiniki kuwa eti ‘uwe mstari wa mbele kuvumbua maovu na mapungufu ya kiutendaji ya mtu ambaye unataka atolewe kwenye nafasi ili wewe uwekwe hapo!’

Kwa namna yoyote ile kama Dkt. Kigwangalla angekuwa anaitaka nafasi ya Uwaziri asingeunga mkono madai ya madaktari. Na kwamba kama kuna mtu ana Taarifa zozote zile zinazoweza kuthibitisha kuwa amekuwa akipanga mikakati ya kutafuta Uwaziri basi aziweke wazi na Mhe. Mbunge atakuwa tayari kujivua nafasi zake zote za uongozi alizonazo.


Mhe. Mbunge anawashauri waandishi wa habari kuwa waandike taarifa ambazo wana uhakika nazo tu na wasikubali kutumiwa na makundi ya wana siasa wenye malengo ya kuchafua wenzao.

Mwisho, mara zote toka mgogoro huu baina ya madaktari na serikali uanze, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) amekuwa akishauri pande zote mbili zikutane, zijadiliane na kutafuta suluhu ya matatizo yaliyopo, na leo hii tena bado anasisitiza kuwa njia pekee sahihi na sawia ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu ni kuzungumza na kuelewana kwenye mambo ya msingi. Hii ndiyo njia pekee itakayoepusha adha kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya, ambao wao ni waathirika wasio na hatia.


Imetolewa Leo Tar 8/Machi/2012 na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega.

Chama cha madaktari (MAT) hakina uwezo wa kisheria kuitisha migomo

Chama cha Madaktari Tanzania ni Chama Cha hiyari na si Chama cha Wafanyakazi ambacho kina UWEZO WA KUITISHA MIGOMO. Kwa mujibu wa masharti ya usajili wa TMA, hakuna kipengele kinachotoa mamlaka kwa MAT kuitisha migomo. Kitendo cha kuitisha migomo ni sababu tosha kwa Msajili wa Vyama vya Hiyari kukifuta Chama hiki ambacho kinaenda nje ya majukumu yake kisheria. Tembelea tovuti ya Chama hiki utakuta kuwa chama hiki kinaongozwa pia na MAADILI (medical ethics). Welcome to Medical Association of Tanzania

“To promote the medical and allied sciences, to maintain the honour and interests of the medical professions and to uphold a high standard of medical ethics and conduct among its members. To act as representative body of the medical profession in Tanzania and to liaise with and advise the Government on health and medical matters. To ensure, maintain and safeguard the interests privileges and welfare of its members.

Moja ya maadili ya madaktari ni kutosababisha madhara kwa wagonjwa.

Kwa sababu uchumi wetu ni wa soko huria, madaktari ambao hawapendi kufanya katika sekta ya umma wawe na ujasiri wa kuondoka na kupeleka huduma zao hospitali binafsi na huko ni soko huria ambalo litawachuja wazuri na wasio wazuri.

Hatua zinazostahili kuchukuliwa:

  1. Msajili wa Vyama vya Hiyari afanye kazi yake na arejee usajili MAT ili ajiridhishe kama MAT bado inastahili usajili kama chama cha hiyari;
  2. Kila daktari ana mkataba binafsi wa kazi. Asiyehudhuria kazini asilipwe mshahara mwisho wa mwezi huu. Kuhudhuria kazini sio kusani kitabu cha mahdhurio na kuondoka;
  3. Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaombe tamko la Mahakama ya Kazi kuwa MAT hawana mamlaka kuitisha migomo na pia madaktari wanaotoa essential services wana utaratibu wa kugoma ambao haukufuatwa.
  4. Madaktari kutoka nchi za nje wanaotaka kufanya kazi Tanzania wakaribishwe na wapewe vibali vya kufanya kazi;
  5. Hatua za Kisheria zichukuliwe dhidi wa wafanyakazi wanaotoa huduma maalum (Essential Services) wanaogoma kinyume na sheria.


Mgomo wa madaktari unahatarisha usalama wan chi yetu kwa sababu sasa unabeba sura ya kisiasa kupitia chama cha hiyari. Hatua zisipochukuliwa, vyama vingine vya hiyari vitafuata mkumbo wa kuvunja sheria. Usalama wan chi uko hatarini pale wenye taaluma na elimu nzuri wanapovunja sheria bila hatua madhubuti kuchukuliwa. MUNGU IBARIKI TANZANIA.

MGOMO MWINGINE WA MADAKTARI TANZANIA WAANZA TENA

Rais wa chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Namala Mkopi ametangaza kuanza kwa mgomo wa Madaktari usio  na ukomo, kote nchini Tanzania.

Mgomo huo unaishinikiza Serikali kuwafukuza kazi Waziri wa Afya Dkt. Hadji Mponda na Naibu Wake Dkt. Lucy Nkya ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya maazimio ya mkutano wao uliofanyika mwezi Februari, 2012 katika ukumbi wa CPL, Muhimbili na Serikali, ikiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

CHADEMA kuzindua kampeni Arumeru Jumamosi kwa maandamano makubwa.

Meneja kampeni wa Mgombea ubunge Jimbo la Arumeru kwa tiketi ya Chadema Vicent Nyerere amesema CHADEMA wanatarajia kuzindua kampeni zao rasmi Jumamosi asubuhi ambazo zitazinduliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.Alisema kuwa uzinduzi huo utakwenda sambamba na maandamano makubwa yatakayotokea Arusha mengine yatatoka KIA na yote yatakutana eneo la Usa River katika viwanja vya eneo la mkutano.



“Mkutano huo utazinduliwa kwa kishindo kwa helkopta, magari, baiskeli na pikipiki, vyote vikiwa vinapeperusha bendera za Chadema, hivyo nawaomba wapenzi wa Chadema wafike eneo husika mapema kushuhudia uzinduzi huo,” alisema Nyerere.Alisema kutokana na maandalizi waliyofanya na jinsi chama chake kinavyoungwa mkono jimbo hilo wanatarajiwa yatakuwa ni maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa katika mkoa wa Arusha.



Nyerere alisema kuwa Chama chao kitafuata taratibu zote za sheria ya maandamano kwa kuelekeza wafuasi wao kutii amri ya barabarani kwa kutembea upande mmoja wa barabara na kuyaachia magari kupita na kumaliza mikutano yao kwa wakati uliopangwa wa kumalizika kwa kampeni za uchaguzi.

Tuesday, October 4, 2011

CHADEMA:TUTAIFIKISHA CCM MAHAKAMANI

CHASEMA SHERIA, MAADILI,TARATIBU VILIKIUKWA, MUKAMA WA CCM ALIA NA WASIMAMIZINeville Meena, Igunga
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kwamba kitapinga mahakamani, matokeo ya ubunge wa Jimbo la Igunga ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu.Katika taarifa yake kuhusu uchaguzi huo aliyoitoa jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alidai kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria, taratibu na maadili katika uendeshaji wake.

Hata hivyo, Mbowe alisema licha ya kupoteza jimbo hilo, chama chake kinajivunia mafanikio makubwa kilichopata katika muda mfupi kwa kupata kura nyingi ikilinganishwa na CUF ambacho licha ya kuwa na mtaji wa kura 11,000 kilizopata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kiliambulia kura 2,014.

Dk Kafumu alishinda kwa kupata kura 26,484 kati ya kura 52,487 halali zilizopigwa, sawa na asilimia 50.4, akiwashinda wenzake saba wa vyama vingine.

Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye wa Chadema alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.3 akifuatiwa na Leopold Mahona aliyepata kura 2,104 sawa na asilimia nne.

Akizungumzia nia yake ya kwenda mahakamani, Mbowe alisema CCM kilitumia kiasi kikubwa cha fedha na rasilimali nyingine katika uchaguzi huo kuliko ambavyo imewahi kutokea katika chaguzi nyingine ndogo na kwamba kulikuwa na hujuma za wazi zilizofanywa, hivyo kukiukwa sheria na maadili yanayoongoza uchaguzi.

Alisema kulikuwa na vitendo vya rushwa vilivyofanywa na chama kimoja cha siasa na kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilishindwa kuchukua hatua licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo kisheria.

Mwenyekiti huyo wa Chadema pia aliilaumu polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akidai kwamba wamechangia kuharibu mchakato mzima wa uchaguzi huo mdogo.

Alidai kwamba CCM kilitumia chakula cha msaada kwa waathirika wa njaa kama silaha ya kisiasa kwenye uchaguzi na kwamba wananchi wa Igunga walipewa mahindi wakirubuniwa ili wakipigie kura chama hicho.

Viongozi wa Serikali
Mbowe alisema ushindi wa CCM pia ulichangiwa na chama hicho kupuuza sheria za uchaguzi kwa kutumia viongozi na rasilimali za umma kwa ajili ya kukinufaisha.

“Mawaziri na viongozi kadhaa waandamizi wa Serikali walifanya kampeni za waziwazi kwa niaba ya CCM na kwa kutumia magari na muda wa Serikali… viongozi haohao wa Serikali walitumia rasilimali za Serikali kama chakula cha msaada, ahadi ya kiserikali kuhusu mgawo wa fedha za ujenzi wa daraja na ahadi ya kutoa pembejeo kwa wakulima,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Mbowe.

Kuhusu NEC, alisema kulikuwa na ukiukwaji wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kutokana na Tume hiyo kuwanyima haki ya kupiga kura baadhi ya watu ambao utambulisho wao ulikuwa na utata.

“Mpigakura yeyote ambaye utambulisho wake ni wa mashaka, anatakiwa aruhusiwe kupiga kura baada ya kupewa onyo na kujaza tamko la kisheria kuthibitisha kuwa ana haki ya kupiga kura katika kituo husika,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Licha ya msimamo huo wa kisheria, NEC ilitoa maelekezo kwa maandishi kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura yanayokataza wapigakura wasiokuwa na kadi za kupiga kura, kutoruhusiwa kupiga kura.”

Alisema mbali na kukiuka Sheria ya Uchaguzi, maelekezo hayo yalitoa mwanya wa ununuzi wa kadi uliofanywa na chama cha siasa kimojawapo na kwamba ndiyo chanzo cha watu wachache kujitokeza kushiriki uchaguzi huo, ikilinganishwa na idadi ya walioandikishwa.

Wapigakura walioandikishwa katika Jimbo la Igunga ni 171,019 na waliojitokeza kupiga kura mwaka huu ni 53,672 sawa na asilimia 31.3, kukiwepo ongezeko la asilimia 2.7 ikilinganishwa na idadi ya waliopiga kura mwaka jana ambao walikuwa 49,013 sawa na asilimia 28.6 ya 171,077 waliokuwa wamejiandikisha.

Mbowe alisema kutokana na upotoshwaji wa kisheria uliofanywa na NEC, ipo hatari ya siku za usoni kukatokea madhara makubwa zaidi kwa watu walioandikishwa katika Daftari ya Kudumu la Wapigakura kunyimwa haki yao.
“Kwa rekodi yake hii na kwa sheria za uchaguzi zilizopo, NEC haina tena sifa ya kuweza kusimamia kazi hii muhimu ya kusimamia kura ya maoni itakayopitisha Katiba mpya ya Tanzania. Chadema itafanya kosa kubwa kama itafumbia macho ukweli huu,” alisema Mbowe.

Uchaguzi wa Igunga pia uliwashirikisha wagombea wengine ambao ni Steven Mahuyi (AFP) aliyepata kura 235, Hassan Rutegama (Chausta) aliyepata kura 182, Said Cheni DP kura 76 na Hemed Ramadhani (SAU) kura 63.

CCM walaumu wasimamizi

Kwa upande wake, CCM kimetoa shutuma kali kwa wasimamizi wa uchaguzi vituoni, kikisema kwamba walisababisha kupungua kwa kura zake katika uchaguzi huo.

Juzi, baada ya Dk Kafumu kutangazwa mshindi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alidai kuwa chama chake kingeweza kupata ushindi mkubwa zaidi lakini kilihujumiwa na wasimamizi ambao alidai kuwa wengi walikuwa na mapenzi kwa Chadema.

“Ushindi huu unaonyesha kwamba kuna uongozi mpya ndani ya nyumba. Tumefanya vizuri lakini kama si hujuma za wasimamizi tungeshinda kwa kishindo kikubwa zaidi,” alisema Mukama.

Tuhuma hizo za Mukama kwa wasimamizi zinatokana na matokeo ambayo yanaonyesha kuwa licha yaa kushinda, CCM kimefanya vibaya katika jimbo hilo ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka jana wakati mgombea wake, Rostam alipopata ushindi wa kura 35,674 sawa na asilimia 72.7 ya kura halali zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mgombea wa CUF, Mahona ambaye alipata kura 11,321 sawa na asilimia 23.1.

Kauli ya Mukama haikuwa ya kwanza kutolewa na viongozi wa CCM dhidi ya wasimamizi kwani siku ya uchaguzi, Oktoba 2, mwaka huu, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje wa chama hicho January Makamba alitoa tuhuma kama hizo akidai kwamba baadhi ya wasimamizi walikuwa wakiwapa wapigakura karatasi za kupigia kura ambazo tayari zilikuwa na alama ya tiki kwa mgombea wa Chadema.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Igunga, Protase Magayane alipuuza tuhuma hizo akisema kuwa kulikuwa na fursa kwa vyama na umma kwa ujumla kutoa pingamizi pale wa wasimamizi hao walipoteuliwa kwa mara ya kwanza.

Alisema vyama vya siasa vilipaswa kufanya mapitio ya makini katika orodha ya wasimamizi na kwamba hatua zingechukuliwa kabla ya uchaguzi, badala ya kusubiri kulalamika siku ya uchaguzi.

CCM yairushia kombora Chadema
CCM kimeibuka na kudai kuwa vurugu za wanachama wa Chadema ndicho chanzo cha idadi kubwa ya watu kutojitokeza kupiga kura.

Katika uchaguzi huo, idadi kubwa ya watu hawakujitokeza kupigakura kwani kati ya watu 171,019 waliojiandikisha ni 53,672 tu sawa na asilimia 31.3 waliojitokeza Jumapili iliyopita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama hicho ndiyo yaliyokipa ushindi Igunga.

“Ushindi huu ni uthibitisho kuwa mapinduzi makubwa yaliyofanyika ndani ya chama yamezaa matunda na yanaungwa mkono na wananchi na ndiyo maana tumeibuka washindi Igunga,” alisema Nnauye na kuongeza:

“Kutokana na fujo za Chadema, idadi kubwa ya watu haikujitokeza kupiga kura. Uchaguzi huu umeonyesha jinsi Chadema walivyokuwa wabakaji wa demokrasia. Watanzania wanatakiwa kuikataa hali hii, hakuna demokrasia ya namna hii.”

Nnauye alisema kitendo cha CCM kushinda udiwani katika Kata 17 kati ya 22 katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Manyara, Mara, Mbeya, Mwanza, Rukwa, Ruvuma na Sinyanga ni ishara kuwa hicho kinakubalika.

Mapokezi mazito
Nnauye alisema viongozi wakuu wa CCM ambao walikuwa Igunga watafanyiwa mapokezi mazito Jumamosi ijayo, Dar es Salaam.

“Kesho (leo) watapokewa na wananchi mkoani Singida, Oktoba 6, watakuwa Dodoma, Oktoba 7 watakuwa Mkoa wa Pwani na Oktoba 8 watakuwa Dar es Salaam. Tumefanya hivi kwa lengo la kuwashukuru wananchi,” alisema