WAKATI Baba wa Taifa amesema maneno yale “Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM”, sikuwa nimeyaelewa vizuri.
Sasa hivi maneno hayo hata hivyo yanapiga kelele katika mawazo yangu na kuacha mwangwi urindimao katika fikra zangu kila kukicha. Kama tunataka kweli kwenda na kufika kwenye ile nchi ya ahadi mambo kadhaa yanahitaji kutokea yakikihusu Chama cha Mapinduzi.
La kwanza ni kuwa CCM lazima ishindwe katika uchaguzi mkuu ujao na kwa kuanzia lazima ishindwe Igunga. Chama chochote tawala kinapokaa madarakani kwa muda mrefu kinajenga tabia mbili za hatari; moja ni tabia ya kuzoea na ya pili tabia ya ufisadi. Kwenye tabia ya kuzoea chama tawala kitakuja na kila aina ya mipango mizuri kwenye vitabu na kwenye makaratasi; vitazindua miradi ya kuvutia na kuanzisha kila aina ya kampeni. Matokeo yake chama hicho kinabakia kuwa ni chama cha “uzinduzi”.
Mara wamezindua barabara, mara wamefungua jengo fulani, mara wamezindua mradi wa visima vya maji n.k Wao sifa yao kubwa iko katika kuzindua vitu na kupiga picha za uzinduzi na kutamba kuwa mradi waliofungua wa wananchi umegharimu kiasi fulani. Na wananchi ambao wamezoea mambo ya kuzindua hujikuta wakisherehekea uzinduzi wa vitu visivyokoma. Hivyo chama kinakuwa na mazoea ya kuanzisha mambo tu. Sasa kuzindua peke yake hakutoshi lazima kuwa na ufuatiliaji endelevu wa yale yaliyozinduliwa.
Leo hii akipita mtu kufanya tathmini ya miradi mbalimbali ambayo imefunguliwa na serikali (ukiondoa ile ya wafadhili ambayo mara nyingi ina ufuatiliaji wa karibu) utashangaa ji kwa kiasi gani miradi ile imetunzwa kwa kiwango kinachostahili. Hebu mtu atembelee shule tulizozifungua miaka mitatu iliyopita kwa mbwembwe hadi kiongozi mmoja kututambia Bungeni kuwa tunapaa. Je, hizo shule leo zinaonekanaje? Je, bado zina mabati yote, milango na madirisha?
Sasa hiyo ni tabia ya mazoea. Yaani chama tawala kinakuwa na mazoea ya kuanzisha mambo bila ya kuyafuatilia ili kuyamaliza au kuhakikisha yanadumu kwa kiwango kinachostahili. Kwa hiyo kinakuwa chama cha mazoea ya mambo yale yale. Ndiyo maana leo hii maneno ya “kasi mpya, ari mpya, na nguvu mpya” huyasikii tena kwa sababu Chama tawala hakiwezi kuwa na “ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya” kikiwa na tabia ya mazoea!
Tabia ya pili ambayo inatokana na chama kuwa madarakani kwa muda mrefu ni tabia ya ufisadi. Tabia hii ya pili inatokana na hiyo ya kwanza (ya mazoea). Watumishi waliodumu muda mrefu katika chama tawala wanakuwa na mazoea ya kufanya mambo yale yale kwa mtindo ule ule na ni vigumu sana kwa wao kubadilika. Mazoea haya yanaanza kujenga tabia ya kuanza kutumia madaraka, vyeo, na nafasi mbalimbali kujinufaisha wao wenyewe huku wakiendelea kuzindua miradi mbalimbali kana kwamba wanafanya kitu fulani cha kushangilia. Sasa haina maana kuwa hawafanyi kitu ila kile wanachokifanya na kukitangaza kuwa wanafanya ni kiduchu kweli kulinganisha na kile ambacho wangeweza kufanya au wanapaswa kufanya.
Sasa huu ufisadi unatokea taratibu kwa sababu kwa vile wamezoeana na wanajuana inakuwa vigumu kweli kwa wao wenyewe kuwajibishana kiasi kinachostahili. Matokeo yake utakuta kuna tabaka la aina fulani la ufisadi unaokubalika katika jamii.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe akiandika kwenye mtandao maarufu duniani wa Watanzania wa jamiiforums.com ameelezea kisa cha mzee mmoja ambaye alikuwa anatafuta haki yake kutoka kwenye idara moja nyeti ya serikali (TRA). Mzee huyo baada ya kuhangaika kwa muda mrefu alijikuta kila anakokwenda ili aweze kutatuliwa tatizo lake alihitaji kutoa ahadi kuwa mambo yakimuendea basi “awakatie” watumishi waliomsaidia kitu kidogo.
Mzee huyo hakuwa tayari kufanya hivyo. Alipopata nafasi ya kumuelezea Kabwe juu ya suala lake na Zitto alipoamua kuandika barua kwa Waziri Mkuu, Mzee yule kwa mujibu wa Mhe. Zitto akainama na kuniambia, “ Mheshimiwa Zitto (ninamquote hapa maana sipendi kuitwa mheshimiwa) kama ukifanikiwa kunisaidia suala hili, nitakujengea nyumba nzuri Kigoma'”
Sasa Zitto anaelezea mwitikio wake “Kalamu ilianguka kwa kutetemeka kwa hasira; Mratibu wa ofisi yetu alikuwa ananiangalia na akitarajia kuachana na mzee huyu. Nilimtazama mzee huyu na kumwambia 'Baba, hii ni haki yako huna haja kuinunua. Mimi pia hii ni kazi yangu, ninalipwa kuifanya. Sitaki nyumba yako. Sitaki chochote kutoka kwako”
Sasa mtu anaweza kuguswa na mwitikio wa Zitto lakini ukiangalia vizuri mwitiko wake ulipaswa kuwa hivyo. Lakini kubwa zaidi (tukiamini simulizi la Zitto) ni ujasiri wa Mzee huyo mwenye shida pasipo woga, haya wala kufikiria anachosema kutoa “hongo” namna hiyo. Ukiangalia utaona kuwa katika sehemu nyingi za jamii yetu tumezoea mno vitendo vya ufisadi kiasi kwamba wakati mwingine hata hatufikirii mara mbili. Hii inatokeana na kujengeka katika jamii yetu kwa utamaduni wa kifisadi ambao msingi wake ni utawala wa muda mrefu wa chama kimoja.
Sasa, ili mambo yaweze kugeuka ni lazima CCM ishindwe uchaguzi wa Igunga ili hatimaye tuweze kuanza upya kujenga Taifa letu jinsi ile ambavyo tunataka.
Lakini jambo jingine ambalo linatokana na hilo la CCM kupoteza uchaguzi ni kuwa aidha CCM kama ilivyo ishindwe kwenye uchaguzi huo au ilazimishwe kushindwa toka ndani yake yenyewe.
Kuilazimisha kutoka nje ni kwa kutokea chama kingine ambacho siyo tu kina sera nzuri lakini wananchi wanaweza kuamini kuwa kinaweza kweli kuchukua madaraka ya nchi na kesho wake wananchi wakaenda zao sokoni, kazini, na shuleni kama kawaida pasipo kukaa na kusikiliza redioni nini kimetokea.
Njia hii ya kuwa na chama mbadala ni bora zaidi na ya kuaminika zaidi kwani italeta nchini siasa mpya ambapo wananchi wanaweza kubadilisha vyama hivi pasipo kuwa na matatizo yoyote au kufikiria mara mbili kwani wanajua vyote viwili vinaweza kuunda serikali na kushikilia nchi.
Mfano mzuri ni uchaguzi wa Marekani ambapo chama cha Repablikani kimepoteza nafasi ya Urais, na mabaraza yake mawili ya Uwakilishi kufuatia ushindi wa Seneta Barack Obama.
Kwa sababu Wamarekani hawana hofu nani anayechukua madaraka kila baada ya miaka minne kwani wanajua akiwazingua wanamtimua miaka minne ijayo! Katika Tanzania bado hili ni gumu kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Kenya na Zimbabwe. Hivyo, hili la kuwa na chama mbadala ni muhimu sana kama kweli tunataka kujenga utawala wa kidemokrasia, huu utitiri wa vyama tulionao unapoteza muda, unatawala vipaji, na kamwe hautaleta chama mbadala. Lakini kuombea hilo kwa sasa ni sawa na kusubiri mvua za masika jangwani!
Ambalo linapaswa kutokea ni kile ambacho kinatokea Afrika ya Kusini sasa hivi. Chama cha Mapinduzi ni lazima kimeguke kama kweli kinataka kurudi kwenye misingi yake na kushiriki upya katika ujenzi wa taifa jipya la Kitanzania kwani kilivyo sasa kinakwenda kwa kuvutana kamba.
Ili kiweze kumeguka kweli kinahitaji ndani yake watu watakaogongana kimawazo na kimtazamo. Ni lazima utokee mgongano wa kifikra, kiuongozi, na kimwelekeo ili CCM iweze kuwa na kambi kubwa mbili ambazo haziwezi kukaa pamoja na hazipaswi kukaa pamoja. Kule Afrika ya Kusini baada ya kambi ya Zuma kujipanga vizuri na hatimaye kumnyima Mbeki uenyekiti wa ANC na baadaye kuhakikisha kuwa Mbeki anakuwa dhaifu ndani ya Chama hatimaye waliweza kusababisha Mbeki kuachia ngazi mapema kabla ya muda wake.
Kama kina Zuma walitarajia Mbeki angeondoka kimya kimya walifanya makosa na matokeo yake mashabiki wa Mbeki wameamua kujimega kutoka ANC na kuunda chama kingine cha kisiasa.
Sijui ni kwa kiasi gani chama hicho kitakuwa na nguvu katika siasa za Afrika Kusini kwani yawezekana kukawa na mambo ya kikabila au majimbo ndani yake lakini kwa vyovyote vile kunailazimisha ANC aidha kubadilika au kujikuta inabadilishwa.
Hilo ndilo linalohitajika kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Hata hivyo haliwezi kutokea hadi pale baadhi ya “vigogo” wa chama hicho hasa wakongwe au wale ambao wamejikuta wakiwekwa pembeni kutokana na misimamo yao watakapoamua kujitoa ndani ya chama hicho na kuanzisha chama kingine. Hili litawezekana tu pale ambapo wakongwe walioko CCM watakapotambua mioyoni mwao kuwa CCM siyo mama yao. Pale watakapotambua kuwa wanaweza wasife wana CCM lakini watakufa wakiwa ni Watanzania!
Sasa hivi heshima kubwa ambayo baadhi yao wanayo (kama alivyosema Mzee Kawawa miaka ile) ni kuhakikisha kuwa wanakufa wakiwa wana CCM pia. Wengine kati yao wameapa kabisa kuwa liwalo na liwe wao ni “wana CCM mpaka kufa”. Nakumbuka wengine wetu tuliimba nyimbo za “naapa naahidi mbele ya Chama, Mapinduzi nitakulinda mpaka kufa”. Lakini ahadi hiyo ni ya uongo kwani utii na mapenzi yetu kama raia wa taifa letu hayawezi kamwe kuwa kwa mtu, idara, taasisi au chama cha kisiasa. Mapenzi na utii wetu wa kwanza na wajuu zaidi ukiondoa ule ulioko kwa muumba wetu ni kwa nchi yetu.
Wazo hili litakapoingia ndani ya viongozi wa CCM hasa wale ambao kweli wanaamini mabadiliko yanahitajika haitawachukua muda kuamua kujitoa ndani ya CCM na kuanza harakati za kuleta mabadiliko ya kweli.
Hili hata hivyo haliwezi kuwa jambo la mtu mmoja mmoja kama ilivyokuwa kwa Ndg. Mrema (mwenyekiti wa sasa wa TLP). Kujiondoa kwa mtu mmoja ndani ya CCM haitoshi inabidi kundi zima la wana CCM mahiri na mashuhuri liamue kujitoa ndani ya chama hicho kama ishara ya kuchoshwa na mambo yalivyo lakini pia kama alama ya kutaka kuanza upya.
Tatizo kubwa la mpango huo ni kuwa kuna dalilii kuwa wale watakaotoka yaweza kuwa ni wale ambao tayari wamekataliwa na wananchi na hawana ule “ujiko” wa kisiasa au mtaji wa kisiasa wa kuwaweza kufanya kuwa na nguvu nchini. Lakini endapo watakaotoka ni wale ambao wananchi wamewaona ni watetezi wao, wapiganaji wao, au kwa namna fulani wanasimamia maslahi ya Taifa basi CCM itakuwa kweli imepata mpasuko unaostahili.
Kumeguka huko kwa CCM kutasababisha mgongano wa kifikra katika taifa, mgongano ambao utachuja makapi na nafaka na kuchuja viongozi uchwara na wenye masihara kutoka katika viongozi walio bora. NI mgongano ambao mbegu zake tumekuta tukizipanda taratibu.
Hakuna kitu ambacho kinaitisha CCM na watawala wake kama wagombea huru. Wagombea huru wasiofungamana na chama chochote ni tishio kubwa kwa CCM kuliko upinzani uliopo sasa. Sababu kubwa ni kuwa wagombea huru hawafungwi na nidhamu ya chama fulani au woga kwa “mwenyekiti wa chama”. Wao wanafungwa na wapiga kura wao. Ni kwa sababu hiyo CCM imejitahidi sana kukwepa kuruhusu wagombea binafsi kwa sababu endapo watafanya hivyo watakuwa wameamua kutumia mafuta yao wenyewe kukaangwa.
Hata hivyo naamini kabisa ya kuwa ni kwa maslahi ya taifa wabunge wa CCM waiteke hoja ya wagombea binafsi na kuilazimisha kwa nguvu ya kisheria. Kama serikali yenyewe haitaki kuleta mswaada wa mabadiliko hayo ya sheria wakati umefika kwa mbunge mahiri wa CCM kuleta mswada binafsi wa kuleta mabadiliko hayo. Sababu kubwa ni kwamba, wakileta mabadiliko ya sheria hiyo ni wazi kuwa wabunge wengi waliopo sasa ndio watakuwa wa kwanza kufaidika nao hasa kama CCM itaendelea kutumia mfumo wake wa kura za maoni na maamuzi ya Kamati Kuu katika kutafuta wagombea wake.
Vinginevyo, bado ninaamini ya kuwa kumeguka kwa chama cha Mapinduzi ni muhimu kutokea ili hatimaye Taifa letu liweze kuanza upya safari ya maendeleo. Sababu kubwa ni kwamba CCM imetawala muda mrefu na haiwezi kubadilika au kujibadilisha.
CCM imeendelea kutawala kwa kawaida huku ukifanya mazingaombwe ya kuonesha inabadilika kumbe inabakia vile vile; na CCM hata kama ikipigiwa mbiu ya mgambo haiko tayari kujisafisha na kuleta mabadiliko ya kweli ya taifa kwa kadiri ya kwamba hali iliyopo inainufaisha yenyewe.
Ndiyo maana utaona kuwa mambo yanayohusu CCM wako tayari kuyadili kwa kina kuyachukulia hatua madhubuti lakini yanapokuja yale yenye umuhimu kwa Taifa inabidi hadi watu waandamane. Hebu fikiria suala la EPA peke yake hadi watu kufikishwa mahakamani lilichukua muda gani?
Na hapo hatujaanza kuangalia suala la Meremeta, Mwananchi Gold, Deep Green Finance, Kagoda, rada, malori, helikopta, majengo ya BoT n.k Kama jambo moja tu limechukua miaka miwili haya yote yakijakumalizwa kuna wengi wetu hapa tutakuwa tumeshaondoka katika ulimwengu huu na wajukuu zetu wakiandalia kuhangaika nayo! Kwa kadiri tunakubali na kushangilia mazingaombwe tunayoyaona ndivyo hivyo na wenyewe hawaoni haraka ya kufanya jambo lolote kwa sababu wamezoea jinsi ilivyo.
Lakini vyovyote vile ilivyo, kama kweli Tanzania inataka kupati nafasi ya kufanikiwa na kuanza kuelekea nchi ile tuitamaniyo, CCM kama ilivyo sasa haistahili kuendelea kuliongoza taifa letu baada ya 2010.
Aidha, wanyang’anywe urais (kama ilivyotokea Afrika Kusini, au wanyang’anywe Bunge (kama ilivyotokea Kenya), au wanyang’anywe vyote viwili (kama ilivyotokea Marekani). Kuwaachia waendelee walivyo sasa, ni kuwapa baraka ya kutudumaza.
|
No comments:
Post a Comment