KATIKA hali isiyo ya kawaida, Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wamerushiana makonde na kusababisha uchaguzi wa meya kuvunjika.
Hatua hiyo ilitokana na baada ya Naibu meya wa halmashauri hiyo, Mariam Dizumba, kudaiwa kuiba kura zilizopigwa na madiwani hao kwenye uchaguzi wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Meya wa halmashauri hiyo, Ally Manya, aliyefariki dunia miezi michache iliyopita.
Kutokana na mapigano hayo baadhi ya madiwani walijikuta wakijeruhiwa na wengine kupoteza simu na vitu vya thamani.Katika uchaguzi huo, ulioanza kwa malumbano makali yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 20 kati ya madiwani wa Chadema na wenzao wa CCM, ambao walikuwa wanajadili jinsi uchaguzi huo utakavyokuwa huru na haki kutokana na upinzani kutosimamisha mgombea.
Kutokana na hali hiyo, Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Nachoa Zakaria, alitoa ufafanuzi wa kanuni za uchaguzi wa nafasi hiyo, huku akiwataka kupiga kura za ndiyo au hapana na kwamba, wapiga kura halali waliojiorodhesha ni 26, akiwamo na Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Baada ya hali hiyo kutulia, Zakaria aliita orodha ya wajumbe na kuwataka kuchukua karatasi za kupigia kura, madiwani wote walipiga kura na kuitwa kuzihesabu.
Zoezi la hesabu lilipomalizika, Naibu meya Dizumba alilisimama na kuanza kutangaza matokeo, akitaja mgombea pekee wa CCM, Charles Mhagama, alipigiwa kura za ndiyo 14 na hapana 12.
Dizumba alisema kutokana na matokeo hayo, Mhagama ndiye meya mpya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.“Naomba msimamizi wa uchaguzi umwite Diwani Mhagama avae joho la Umeya na kukalia kiti chake,” alisema Dizumba.
Baada ya Msimamizi kumwita Mhagama na kumtaka kuvaa joho la Umeya, baadhi ya madiwani walimtaka msimamizi kuhesabu upya kura hizo ili madiwani wote washuhudie.
“Naomba msimamizi usitishe zoezi la kumtaka Diwani Mhagama akalie kiti cha Umeya, kwa sababu kuna mashaka makubwa na zoezi la utangazaji matokeo, hivyo zihesabiwe kura upya na madiwani wote wazione,” alisema Diwani wa Kata ya Mfaranyaki, Seneta Yatembo.
Wakati wakiendelea kuzozana, Diwani wa Viti Maalum (Chadema), Rhoda Komba, akawaita madiwani wenzake kushuhudia Dizumba alivyokuwa anaiba kura zilizopigwa za hapana kutoka kwenye sanduku la kura, huku akichukua kura za ndiyo kutoka kwenye mkoba wake kuziweka ndani ya sanduku.
Hali hiyo ilisababisha vurugu kubwa na kumfanya Dk Nchimbi (ambaye ni WAZIRI wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo) kukimbia na sanduku la kura kuelekea nje ya ukumbi, kabla ya kunyang’anywa na kutakiwa kulirudisha ndani na madiwani wakiongozwa na wenzao wa Chadema.
Baada ya tafrani hiyo, madiwani wa Chadema waliitisha kikao na waandishi wa habari na kutoa tamko la kutomtambua Mhagama kuwa meya na kwamba, wameomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuitisha uchaguzi mwingine. Chadema ina madiwani saba na CCM 20.
Kwa upande wa madiwani wa CCM, walisema walichofanya wenzao wa Chadema kwa kufanya fujo na kutaka kuwapiga wengine ni kitendo kibaya, kukuza demokrasia.
SOURCE:Mwananchi
No comments:
Post a Comment