Monday, September 26, 2011

Kuku Unaowafuga Mwenyewe Wanapokukataa! ( Makala, Raia Mwema)

 Na Maggid Mjengwa,

KUNA kisa cha bwana mfuga kuku aliyeshangazwa kwa kuku wake mwenyewe aliowafuga kumkataa. Alishangaa iweje kuku aliokuwa akiwapa pumba na mtama, wakala wakashiba, kisha waje wamwandame na hata kumparura.


Na mwanadamu unafanyaje unapofikwa na hali ya kuku wako unaowafuga mwenyewe kukukataa? Mwingine atajibu kwa haraka; ” nitawachinja!”
Hilo ni jibu la mtu mpumbavu; maana mwanadamu hafugi kuku ili awachinje wote kwa siku moja. Mbali ya kitoweo, anahitaji kuku wamtagie mayai na wamtotolee vifaranga wapya; hivyo basi, wamuinulie kipato chake.

Mwanadamu afanye nini basi?
Ndio, kwa mwanadamu, ukiona hata kuku wako unaowafuga wanakukataa, basi, kaa chini utafakari kwa kina. Kuna tatizo. Na tatizo si kuku, ni lako mfuga kuku. Yumkini banda la kuku unaowafuga halina madirisha ya kuwapa hewa na mwanga. Na siku zote, kuku hawabanani ila ni mwenye kuku ndiye anayewabana kuku wake. Na hata kuku hufikwa na ukomo wa kustahimili kubanwa.


Mwezi Februari mwaka huu niliandika katika safu yangu hii kuhusu kilichokuwa kikitokea katika nchi za Kiarabu ikiwamo Misri. Niliandika kuwa yanayotokea Misri na kwingineko iwe fundisho kwa Chama tawala Tanzania, CCM. Na nikasema kuwa mabadiliko yanakuja hata katika nchi zetu hizi, na kuwa tungeziona ishara.


Maana; tuliona kule Misri kuwa Wamisri wale walifikia ukomo wa uvumilivu wa kukandamizwa. Wakaingia mitaani kuandamana kwa mamilioni hata wakamtimua Hosni Mubarak madarakani.
Waarabu wale walikuwa na kiu ya uhuru, kiu ya haki . Ni kiu ya zaidi ya miongo mitano, miaka 50. Kule Misri, tuliwaona Wamisri wenye furaha kuu usiku ule wa mkesha wa ’Tahrir’; neno lenye maana ya ukombozi.


Wamisri walikesha wakiimba na hata kutoa machozi ya furaha. Misri, kama ilivyokuwa kwa Tunisia na juzi hapa Libya, hatukuziona bendera za vyama. Tulizoziona ni bendera za mataifa hayo.
Kwao, ilikuwa ni sawa na mataifa yao kuzaliwa upya. Niliandika kuwa, furaha ile ya Wamisri ni sawa kabisa na taifa lao kushinda kwa mara ya tano fainali za Kombe la Dunia.

Wamisri wale hawakuchoshwa tu na Hosni Mubarak. Walichoshwa na mfumo mzima na hususan chama chao tawala. Ndio, tulishuhudia, kuwa jengo la kwanza kutiwa kiberiti na waandamanaji lilikuwa ni jengo la Makao Makuu ya Chama tawala cha nchi hiyo cha NDP - National Democratic Party. Kilikuwa chama kikongwe na kilichoshika hatamu za uongozi.


Kwa Wamisri, NDP kilikuwa ni chama walichokihofia hata katika maisha yao ya kila siku. National Democratic Party kwa maana ya Chama Cha Taifa Cha Demokrasia hakikuwa cha Taifa na wala Demokrasia ndani yake. Kilikuwa chama cha wateule wachache akiwemo mwana wa Hosni Mubarak aitwaye Gamal Mubarak. Mwana huyu wa rais alipewa cheo cha ukatibu mkuu na aliandaliwa na baba yake kumrithi madaraka ya urais.


Ndio, Wamisri walifikia ukomo wa uvumilivu. Vijana wale wa Tunis, Cairo, Tripoli na Benghazi hawana tofauti na vijana wa Kigali, Nairobi, Dar es Salaam na Kampala. Tofauti ni kwenye viwango vya uvumilivu.
Ni kama kabati la nguo. Kabati likijaa nguo, na mwenye nalo akazidi kuweka nguo, basi, sio tu mwenye nalo atashindwa kulifunga, bali nguo zitaanza kuanguka.

Makabati ya vijana wa Tunisia , Misri na Libya yalishajaa. Ndio maana tumewaona vijana wale wakilala mbele ya vifaru vya jeshi . Walikuwa tayari kwa lolote liwalo na liwe. Makabati ya vijana wetu bado yana nafasi ya kuweka nguo. Busara kwa watawala wetu ni kutosubiri yajae.


Ndio, binadamu anayekandamizwa sana hufikia kikomo cha uvumilivu. Miaka kumi iliyopita hakuna aliyefikiri vijana wale wa Tunisia, Misri na Libya wangefanya waliyoyafanya.
Yaliyotokea Misri, Tunisia na Libya ni darasa kubwa kwa watawala na vyama barani Afrika kuwa unapoukandamiza mpira uliojaa na ukabonyea, basi, kuna matokeo ya upepo kupungua, mpira kufutuka upande mwingine au kupasuka. Mawili ya mwisho ni lazima yatokee, ni suala la wakati tu.


Viongozi Afrika wanapaswa kutambua sasa kuwa Mwafrika wa mwaka 1975 si Mwafrika wa mwaka 2011. Waafrika wameamka. Viongozi Afrika wana lazima ya kuendana na mabadiliko ya wakati. Hizi ni zama za mabadiliko. Na Mabadiliko ya amani Afrika yanawezekana, mwenye kuyazuia mabadiliko ya amani, atambue, kuwa mabadiliko yenye vurugu hayaepukiki. Hilo la mwisho lina hasara kubwa.

CCM ina cha kujifunza?
Ni ukweli, idadi ya Watanzania, na hususan vijana waliokichoka Chama tawala, Chama cha Mapinduzi inaongezeka kila kukicha. Kufikiri kingine ni kujidanganya. Leo kuna vijana wenye kiu kubwa ya kuiondoa CCM madarakani ili waone tu itakuwaje wakija wengine. Maana, CCM pia imejitengenezea mazingira ya kuhofiwa badala ya kuheshimiwa.


Mathalan, kuna wengi leo wananing’iniza bendera za CCM kwenye biashara zao au kujiita wana CCM si kwa sababu wanakipenda na kukiheshimu chama hicho; bali wanakihofia.
Ni ukweli leo kuna Watanzania wenye kukihofia zaidi Chama Cha Mapinduzi kuliko Mungu wanayemwabudu. Na lipi jema kwa mtawala na chama; kuhofiwa au kupendwa? Mwingine angependa vyote, lakini haiwezekani. Jema ni kupendwa na kuheshimiwa.


CCM itambue sasa kuwa, mabadiliko yanakuja hata Tanzania. Ni suala la wakati tu. Na vijana wa Tanzania huenda wasiingie mitaani wakafanya kama wenzao wa Misri, Tunisia na Libya. Watasubiri siku ile ya kwenda kupiga kura ifikapo 2015. Hilo la subira ya vijana ndilo tunaloliombea.


Na huku mitaani tunawasikia vijana wengi wa Kitanzania wenye kuisubiri kwa hamu 2015. Yumkini wamedhamiria kuandamana kwa wingi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura. Wataandamana kwenda vituo vya kupigia kura kwa nia ya kuiondoa CCM madarakani kwa nguvu za kura.

Salama ya CCM?
Ni ukweli kuwa CCM ina hali ngumu kuelekea 2015. Chama kimepoteza mvuto kwa kundi kubwa la vijana. Anayesoma kwa makini alama za nyakati anaweza kuona kuwa CCM ikiwa na bahati inaweza kwa tabu kutoa rais 2015, lakini, takribani nusu ya wabunge wa bunge lijalo watatoka kambi ya upinzani. Na itakuwa miujiza kama rais wa 2020 atatoka CCM.


CCM ijiandae sasa kuwa chama cha upinzani. Na inaweza kubaki hai kwa muda mrefu kama itaipitisha nchi hii kwenye Katiba itakayoifanya Tanzania kuwa nchi ya kisasa zaidi. Yawepo mazingira ya uwezekano wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Maana; kwa Katiba ya sasa, CCM ikitoka madarakani, basi, yaweza pia ikawa ndio mwisho wake; maana chama hicho kitakufa.


Na CCM ya sasa inahitaji ‘Tahrir’ yake ya ndani ya chama. Nimepata kuandika kuwa ili CCM isalimike na kubaki madarakani katika chaguzi zijazo, sio tu inahitaji kufanya mabadiliko makubwa; bali mabadiliko makubwa yenye kishindo.


CCM inahitaji kurudi kwenye misingi iliyoanzisha chama hicho. Huu ni wakati wa kurudisha misingi ya kimaadili ya chama na uongozi. Misingi iliyokuwapo huko nyuma. Angalia, iko wapi Miiko ya Uongozi? Imevunjwa, na ndio maana ufisadi umetamalaki.


Kwa mwana CCM, sasa sio suala la kushinda uteuzi wa ndani ya Chama na kujihakikishia kuingia Ikulu au Bungeni, kuna umma unaotaka mabadiliko utakaomkabili mgombea wa CCM - awe mgombea urais, udiwani au ubunge. Kuingia ulingoni na ‘CCM ile ile’ itakuwa ni hatari kwa wagombea wengi wa CCM siku zijazo.


Ni ukweli, kuwa ndani ya CCM imeanza kuporomoka, misingi iliyopelekea kuanzishwa kwa Chama hicho tukianzia na vyama mama vya TANU na Afro- Shiraz. Hili ni jambo la hatari sana. Ikumbukwe, vyama mama kwa CCM, TANU na Afro- Shiraz, vilikuwa ni kimbilio la makabwela, kimbilio la wanyonge.


Lakini CCM ya sasa inakimbiliwa na wafanyabiashara, wasomi na wajanja wengine. Wasomi hapa kwa maana ya hata wale wenye taaluma zao. Wako tayari kuzikimbia taaluma zao na kuingia kwenye siasa za vyama, hususan Chama cha Mapinduzi. Baadhi yao wanasukumwa huko kwa ajili ya kutafuta maslahi zaidi. Maslahi binafsi. Na kuna wanaoambiwa; "Mkitaka mambo yenu yawanyokee, njooni CCM". Si mambo ya wananchi, ni mambo yao binafsi!


Kuna wanaokimbilia ndani ya CCM kwa kuamini katika malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa chama hicho. Lakini kuna wanaokimbilia ndani ya CCM wakiwa na malengo na madhumuni ya kwao binafsi yasiohusiana kabisa na ya CCM. Kwao wao, CCM ni sawa na daraja la miti la kuwasaidia kuvuka na kufika wanakotaka kwenda.


CCM ina nafasi ya kujisahihisha. Ianze kazi hiyo sasa. Nahitimisha.
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo

No comments:

Post a Comment