Thursday, September 22, 2011

CHADEMA 74%-IGUNGA

•  Kapteni Komba, Mukama nusura washikane mashati

na Mwandishi wetu
WAKATI zikiwa zimesalia wiki takriban mbili kabla ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga, timu ya kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) imesambaratika, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Wakati CCM ikisambaratika, tathmini ya awali ya uchaguzi iliyofanywa jimboni humo, inaonyesha kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitaibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 74 ya kura zote.
Tathmini hiyo ambayo imefanywa na CHADEMA kwa kuwashirikisha wanazuoni na baadhi ya wanahabari kwa takriban wiki tatu, imetumia takwimu za maeneo ya vijijini na mjini Igunga.
Habari zaidi zinasema CHADEMA imefanya uchambuzi na kuweka mikakati makini ya kudhibiti mianya yote ya hujuma, kwa kuwatumia makada wake na baadhi ya wana CCM na wananchi wanaojitolea, wasioridhishwa na mwenendo wa jumla wa chama tawala jimboni humo.
Nguvu hiyo ya CHADEMA ndiyo imesababisha baadhi ya wanachama na makada wa CCM kuvujisha taarifa za hujuma zilizomhusisha Mkuu wa Wilaya, Fatuma Kimario, na mabalozi wa nyumba 10 waliokamatwa na vijana wa CHADEMA na kuwekwa chini ya ulinzi.
Baadhi ya makada maarufu wa CCM wanasema wameshakata tamaa na kwamba mbinu pekee inayoweza kukiwezesha chama chao kushinda ni nguvu ya dola; si sanduku la kura.
Hata hivyo, walionyesha wasiwasi kwamba jinsi CHADEMA walivyojiandaa, hata hizo nguvu za dola zinaweza zisifue dafu, kwani makundi yaliyo ndani ya CCM ndiyo yanayoelekea kukiongezea CHADEMA nguvu na kukipa ushindi.
Habari zaidi kutoka Igunga ambako kampeni za vyama vya siasa zimeshika kasi, zinasema kuwa timu ya kampeni iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Mchemba, imesambaratika hasa baada ya Mchemba kukumbwa na kashfa ya fumanizi na mke wa kada mwenzake wa CCM.
Habari kutoka ndani ya CCM Igunga na Ofisi Ndogo ya Makao Makuu jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa kuna shinikizo kutoka ndani ya chama hicho kutaka Mchemba aondolewe kwenye kampeni hizo, kwa madai kuwa kashfa ya fumanizi inaweza kuwavurugia kampeni zao.
Kwa mujibu wa habari hizo, tangu kuibuka kwa kashfa hiyo, timu ya kampeni ya CCM imegawanyika.
Wapo wanaotaka Mchemba aondolewe kwenye kampeni, lakini pia wapo wanaotaka aendelee.
Kusambaratika kwa timu hiyo ya kampeni kumetokana na uchunguzi wa CCM wa hivi karibuni ambao ulibaini kuwa timu hiyo haiko kitu kimoja.
“Timu yetu ya kampeni Igunga haiko kitu kimoja, na hata taarifa za kashfa ya kuwa meneja wetu wa kampeni ana uhusiano usiofaa na mke wa kada mwenzake wa CCM, zilisambazwa na kundi la vijana wa CCM wasiotaka jimbo hilo libaki CCM,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CCM inaamini kuwa kundi hilo lililoasi ndani ya CCM, lilipanga mkakati huo na kuhakikisha kigogo huyo wa CCM ananaswa na kukisababishia chama hicho kukosa ushindi.
Duru za siasa kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa inashangazwa na kila mkakati unaofanywa kwa siri na chama hicho, umekuwa ukinaswa na wapinzani wao katika mazingira ambayo wanaendelea kuyafanyia utafiti ili kuwaengua baadhi ya wajumbe walioko ndani ya timu ya kampeni.
Wiki iliyopita, timu hiyo ya kampeni ya CCM, iliingia katika msukosuko mkubwa baada ya Mwingulu, anayeongoza kampeni hiyo, kudaiwa kufumaniwa na mke wa mtu.
Inadaiwa kuwa sakata hilo lilianza baada ya mume wa mwanamke anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kigogo huyo kuvamia chumba ambacho watuhumiwa hao walikuwamo na kuanza kumwadhibu mkewe kwa kipigo.
Wakati vuta nikuvute kati ya mke na mume ikiendelea chumbani, kigogo huyo wa CCM alifanikiwa kutoroka na kuwaacha wanandoa hao ambao wote wawili ni makada wa CCM, wakiendelea kupambana.
Mtafaruku huo ulimsababishia mwanamke huyo aliyekuwa miongoni mwa kundi la mabinti wapatao 10 wanaotumika kuhamasisha kwenye kampeni hizo kupata majeraha makubwa yaliyomlazimisha apelekwe hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Kabla ya kwenda hospitalini, mwanamke huyo alilazimika kupita katika kituo cha polisi cha Igunga ili akapatiwe fomu maalum ya idhini ya matibabu (PF3).
Wakati nje ya uwanja wa kampeni mambo yakiwa hivyo, CCM mwishoni mwa wiki ilikuwa na kikao maalum kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Willson Mukama, kufanya tathmini ya namna kampeni zao zinavyoendeshwa na mbinu za kukabiliana na wapinzani wao, hasa CHADEMA, ambao wameonekana kuwa na mvuto zaidi.
Wajumbe wengine waliokuwa kwenye kikao hicho ni baadhi ya wajumbe wa sekretarieti, pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Philip Mangula, na kiongozi wa kundi la sanaa za maonyeshola la CCM la Tanzania One Theatre (ToT), Kapteni John Komba.
Habari ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa kilikuwa na mvutano mkubwa hasa kati ya Kapteni Komba na Mukama kuhusu namna ya kuendesha kampeni hizo.
“Kapteni Komba aliwasilisha taarifa yake ya kutaka aongezewe fedha kwenye kundi lake la ToT, tofauti na fedha wanazolipwa sasa ambazo alisema hazitoshi, Katibu Mkuu alikuwa hataki kuongeza hata senti tano. Hapo palikuwa hapatoshi. Mzozo ulikuwa mkali sana,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho mjini Igunga.
Habari hizo zilizema kuwa mzozo huo ulimalizwa na Mangula ambaye naye ameletwa mjini hapa kuimarisha kampeni za CCM ambazo tathmini iliyofanywa ndani ya chama hicho inaonyesha kuwa wanaweza kushindwa vibaya kwenye uchaguzi huo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kundi la TOT, lina hali mbaya kifedha na hivi sasa limeamua kufanya maonyesho ya kiingilio cha fedha kila mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu.
Uchaguzi mdogo katika jimbo hilo lililoachwa wazi na Rostam Aziz (CCM), aliyejiuzulu unatarajiwa kufanyika Oktoba 2 ambapo vyama vinane vya siasa vinashiriki
SOURCE:TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment